Nge-mjeledi vibete (kutoka Kiing. microwhip scorpion) ni arithropodi wa oda Palpigradi katika ngeli Arachnida wafananao na nge-mjeledi wadogo kabisa. Kwa kadiri urefu wao ni mm 1-1.5 na mm 3 ni urefu mkubwa kabisa. Kama arakinida wote wana miguu minane, lakini jozi ya kwanza imekuwa kama maungo ya hisi. Kwa upande mwingine pedipalpi hutumika kwa kutembea, kwa hivyo inaonekana kama wadudu hawa wana miguu kumi. Mjeledi wa jina lao ni aina ya mkia mrefu na mwembamba wenye manyoya; urefu wake uneweza kuwa sawa na urefu wa kiwiliwili. Kama kawaida kiwiliwili kina sehemu mbili: kefalotoraksi (cephalothorax: kichwa na kidari) na fumbatio. Nge-mjeledi vibete hawana macho na kwa kawaida hawana maungo ya kupumua; hupata oksijeni kupitia kutikuli (“ngozi”) yao kwa ajili ya ukubwa wao mdogo sana. Lakini spishi kadhaa zina vifuko fumbationi vinavyofanana na mapafu. Wadudu hawa huishi katikati ya chembe za ardhi ambapo hula vijidudu na viani.
Makala hii kuhusu "Nge-mjeledi kibete" inatumia neno (au maneno) ambalo si kawaida na matumizi yake ni jaribio la kutafsiri neno (au maneno) la asili microwhip scorpion kutoka lugha ya Kiingereza. Neno (au maneno) la jaribio ni nge-mjeledi kibete.Kamusi za Kiswahili ama zinatofautiana kuhusu matumizi ya neno hili au hazieleweki au hazina neno kwa jambo linalojadiliwa.