dcsimg

Hinabuluu ( Swahili )

provided by wikipedia emerging languages

Hinabuluu ni ndege wa ardhi wa familia Pittidae. Ndege hawa ni wakubwa na wanene kiasi wenye miguu mirefu, mkia mfupi sana na domo lenye nguvu. Spishi nyingi zina rangi kali. Wanatokea ardhini kwa misitu minyevu ya tropiki ya Afrika, Asia na Australia. Hula makoa, wadudu na wanyama wengini kama wale. Hujenga tago la mviringo kwa manyasi na majani lenye mwingilio kwa upande wake. Jike huyataga mayai 4-5.

Maelezo

Hinabuluu ni ndege wadogo hadi wakubwa kiasi ambao ukubwa wao unaenda kutoka hinabuluu milia-buluu aliye na sm 15 hadi hinabuluu mkubwa ambaye anaweza kufikia urefu wa sm 29. Wana uzito wa g 42 hadi 210. Wana mwili imara na tarsusi ndefu zenye nguvu (mifupa ya chini ya mguu) na miguu mirefu. Rangi ya miguu na vidole inaweza kutofautiana sana hata ndani ya spishi. Hii inaweza kuwa tabia inayotumiwa na majike katika kuhukumu ubora wa mwenzi atakayependa. Mabawa yana manyoya makuu kumi yaliyoviringa na yaliyo mafupi kwa kawaida; yale ya spishi nne zinazohamahama yamechongoka zaidi. Kuna manyoya tisa ya kufuata na lile la kumi ni dogo. Kitabia kinabuluu husita kuruka lakini wana uwezo na hata nguvu ya kuruka. Mkia ni mfupi hadi mfupi sana na hujumuisha manyoya kumi na mawili.

Kinyume na spishi nyingi za ndege wa sakafu ya msitu, manyoya ya hinabuluu mara nyingi yana rangi kali. Spishi moja tu, hinabuluu masikio, ina rangi za kujificha kenyekenye kwa wapevu wa jinsia zote mbili. Katika jenasi hiyo hiyo, Hydrornis, kuna spishi tatu nyingine zilizo na manyoya yenye rangi hafifu kuliko manyoya ya wastani, hinabuluu kisogo-buluu, hinabuluu kiuno-buluu na hinabuluu kisogo-kutu. Kama hinabuluu wengine wa Hydrornis wana manyoya tofauti kulingana na jinsia, majike wakiwa na rangi hafifu na kujificha zaidi kuliko madume. Kwa kawaida jinsia katika familia hiyo huwa kufanana sana ikiwa siyo sawa kabisa. Katika takriban familia nzima rangi kali huwa kuwako upande wa chini na mabaka ya rangi kali kwenye kiuno, mabawa na manyoya wa msingi wa mkia zinaweza kufichwa. Kuwa na uwezo wa kuficha rangi kali kutoka juu ni muhimu kwa sababu mbuai wengi hukaribia kutoka juu. Spishi nne zinakuwa na sehemu za juu zenye rangi kali.

Msambazo na makazi

Kwa ujumla hinabuluu ni ndege wa misitu na maeneo ya vichaka ya kitropiki. Spishi nyingi zinahitaji misitu yenye gubiko jingi, tabaka tajiri la chini, na takataka za majani kwa kusudi la kujilisha, na mara nyingi hupatikana karibu na maji pia. Spishi fulani hukaa katika vinamasi na misitu ya mianzi, na hinabuluu kapa, kama jina lake linavyoonyesha, ni stadi wa kapa. Spishi kadhaa ni stadi wa misitu ya maeneo ya chini. Kwa mfano, hinabuluu upinde-mvua haipatikani juu ya m 400. Spishi nyingine zinaweza kutokea kwenye miinuko ya juu zaidi, kutia ndani, kwa mfano, hinabuluu kisogo-kutu, ambaye amepata hadi m 2,600. Mapendekezo ya mwinuko hutofautiana katika hinabuluu kupendeza ndani ya eneo lake. Anaweza kupatikana hadi m 1,300 nchini Taiwan lakini hukaa miinuko ya chini nchini Japani. Pamoja na mazingira ya asili, hinabuluu wanaweza kutumia mahali palipobadilishwa na binadamu. Kwa mfano, hinabuluu mabawa-buluu na hinabuluu kofia hutumia mbuga na bustani za mijini Singapore.

Miendo ya hinabuluu imefahamika vibaya na kuichunguza ni ngumu sana. Machunguzi ya kuwawekelea ndege koa hayakusaidia kuitambulisha. Katika uchunguzi mmoja nchini Ufilipino hinabulu tumbo-jekundu 2000 waliwekelewa koa lakini ndege kumi tu walikamatwa tena, na mmoja tu wa ndege waliokamatwa tena alikamatwa zaidi ya miezi miwili baada ya kukamatwa mara ya kwanza. Spishi nne tu za hinabuluu ni wahamiaji kabisa au ghalibu, zote katika jenasi Pitta: Hinabuluu Hindi, hinabuluu wa Afrika, hinabuluu kupendeza na hinabuluu mabawa-buluu. Kama vile hizi nne, nususpishi ya kaskazini ya hinabuluu kofia ni mhamiaji kamili. Spishi nyingine hufanya miendo midogo zaidi na ndani ya eneo lao, ambayo haifahamiki vizuri, zinazoshirikisha hinabuluu mpiga-kelele wa Australia. Uhamiaji wa hinabuluu inaonekana kutokea usiku, na hinabulu huhamia katika makundi madogo kejekeje ambayo hutumia mahali sawa pa kupumzika na kujilisha kila mwaka.

Mwenendo na ekolojia

Ujamii na miito

Hinabuluu hukiakia mchana kwa kuwa wanahitaji mwangaza ili kupata mbuawa wao walio na rangi za kujificha mara nyingi. Hata hivyo hupatikana katika maeneo ya giza mara nyingi na hujificha sana, ingawa wataitikia miigo ya miito yao. Kwa kawaida hupatikana kama ndege moja na hata ndege wachanga hawashirikiana na wazazi wao isipokuwa wakilishwa. Jambo la pekee kwa maisha yao ya faragha ni makundi madogo yaliyoonekana wakati wa uhamiaji.

Hinabuluu hupenda kukaa katika eneo lao, na maeneo yana ukubwa kutoka 3,000 katika hinabuluu wa Afrika hadi m² 10,000 katika hinabulu upinde-mvua. Wamepata pia wakiwa na ugomvi sana katika kifungo na hushambulia spishi nyingine na hata wenzao. Mwenendo kama huo haujaonekana mwituni. Hinabuluu watafanya maonyesho ya ulinzi wa eneo kwenye kingo za maeneo yao. Mapigano kati ya wapinzani wametiwa kumbukumbu mara moja tu. Uonyesho mmoja wa kieneo kama hao hufanywa na hinabuluu upinde-mvua, ambaye anaweka miguu yake minyofu na anainamia mpinzani kwenye kingo ya eneo lake akitoa mwito wa kukoroma. Maonyesho kama hayo yanaunganishwa kwa miito iliyotolewa wasipoonwa na wapinzani. Miito hiyo wa kieneo hutolewa mara nyingi na inaweza kujaza hadi 12% ya matendo ya mchana ya ndege. Spishi zinazohamia hutetea maeneo ya kujilisha ambapo hawazai kama vile yale ambapo wanazaa.

Sauti za hinabuluu zinaelezwa vizuri zaidi kama miito, kwa kuwa zina muda mfupi na silabi moja au mbili, na mara nyingi zina sauti ya filimbi au kuvuma. Hufanywa na jinsia zote mbili mwaka mzima. Spishi moja, hinabuluu mweusi-na-mwekundu, pia alielezwa kufanya kelele ya mitambo mwaka 2013. Sauti hii ya kugongagonga ilitolewa wakati wa kuruka na nadharia tete ni kwamba inafanywa na mabawa.

Chakula

Sehemu kubwa sana ya chakula cha hinabuluu ni nyungunyungu wakifuatwa na konokono. Nyungunyungu wanaweza kuwa haipatikani kimsimu katika hali kavu wakati wanapoendelea zaidi kwenye udongo. Hinabuluu pia huchukua mbuawa wengi wa invertebrata wanaojumuisha vikundi vingi vya wadudu kama vile mchwa, sisimizi, mbawakawa, wadudu kama visulisuli, vipepeo na nondo. Kaa wa maji baridi, tangu, majongoo, na buibui huchukuliwa pia. Spishi fulani, kama vile hinabuluu kupendeza na hinabuluu upinde-mvua, wamewekwa kumbukumbu kwa kujilisha kwa mbuawa wadogo wa vertebrata. Hao ni pamoja na mijusi-islam, vyura, nyoka na, kwa kisa cha hinabuluu kupendeza, virukanjia. Pia kuna kumbukumbu za hinabuluu kadhaa wanaochukua chakula cha mimea, kama vile matunda ya mikindu ya Carpentaria au mbegu za mahindi.

Hinabuluu hujilisha kwa mtindo wa mikesha wakisogeza majani kando kwa mwendo wa kufagia wa domo. Pia wameonwa kupekechua udongo mnyevu kwa domo lao ili kutambua nyungunyungu. Wana hisia nzuri ya harufu na kumedokezwa kuwa wanaweza kutambua nyungunyungu kwa njia hii. Dokezo hilo limeegemezwa na utafiti ambao uligundua kuwa hinabuluu Hindi ana tunguu kubwa kabisa la ndege 25 kama shomoro wanaochunguzwa. Spishi nane zimewekwa kumbukumbu kwa kutumia mawe kama fuawe ambazo juu yao koa hupigwa mpaka kuwa wazi ili kuliwa na hinabuluu upinde-mvua ameonwa kutumia mzizi wa mti ili kufanya hiyo.

Uzazi

Kama ndege wengi hinabuluu huzaliana na mwenzi mmoja na kulinda maeneo ya kuzaliana. Spishi nyingi huzaliana kwa kimsimu na kuchagua wakati wa uzazi wao kutokea mwanzoni mwa msimu wa mvua. Mbali na hii ni hinabuluu mrembo, ambaye huzaa takriban mwaka mzima, kwa sababu kisiwa cha Manus ambapo anazaa kinapata mvua mwaka mzima. Mienendo ya ubembelezi ya familia haijulikani vizuri, lakini dansi yenye madoido ya hinabuluu wa Afrika inajumuisha kuruka hewani huku kifua kilichojikuta na kutua mabawa yakitandika na kurudi chini kwenye kitulio.

Hinabuluu hujenga kiota cha msingi ambacho ni kuba lenye mwingilio kwa upande mmoja. Muundo wa kiota una upatano katika familia nzima. Ukubwa wa kiota ni kama mpira wa raga na kwa kawaida hufichwa vizuri kati ya mimea inayotambaa na aina nyingine. Uonekano wa kiota pia ni mgumu kutofautisha kutoka chungu la majani yanayotiwa pamoja na upepo. Spishi chache huunda "mkeka wa mlango" kwa vijiti (wakati mwingine hupambwa na mavi ya mamalia) mbele ya mwingilio. Viota vinaweza kuwekwa ardhini au mitini. Spishi fulani hujenga viota mitini kila mara, kama spishi zote mbili za Afrika. Wengine hujenga viota ardhini tu na wengine huonyesha hitilafu kubwa. Jinsia zote mbili husaidia kujenga kiota, lakini dume anafanya takriban kazi yote. Inachukua siku mbili hadi nane ili kujenga kiota kipya, lakini hii huenda inatofautiana kulingana na uzoefu wa ndege wanaohusika. Kiota kipya hujengwa kwa kila jaribio la uzazi, na kazi ya kujenga kiota kwa uzazi wa pili inaweza kuanza wakati makinda ya uzazi wa kwanza bado wanapolishwa.

Idadi ya mayai hutofautiana kulingana na spishi. Kwa kawaida mayai 3-5 hutagwa, lakini mawili ni kawaida kwa hinabuluu mwekundu, ambapo sita ni kawaida kwa hinabuluu mabawa-buluu na hinabuluu Hindi. Inadhaniwa kuwa spishi za viwango vya juu vya umbuai huwa na mayai machache zaidi, kwa sababu idadi ndogo zinahusisha safari chache za kuleta chakula ambazo zinaweza kumwangamiza mbuai kwamba kiota kiko, na idadi ndogo ni rahisi zaidi kuzibadilisha ikiwa zimepotea. Idadi ya mayai inaweza kutofautiana ndani ya spishi kulingana na latitudo. Uchunguzi wa hinabuluu wapiga-kelele uligundua kwamba ndege katika tropiki walikuwa na idadi ndogo za mayai kuliko wale katika mazingira ya wastani.

Mayai ya hinabuluu yamechongoka kidogo kwa mwisho mmoja na kuwa laini kwa kawaida (mayai yaliyo na vishimo vya kina kikubwa ya hinabuluu mrembo ni hitilafu). Ukubwa wa mayai hutofautiana kulingana na spishi, spishi ndogo zikitaga mayai madogo zaidi. Pia kuna hitilafu katika ukubwa wa mayai ndani ya spishi katika spishi zilizo na maeneo makubwa. Kwa mfano, mayai ya hinabuluu wapiga-kelele ni madogo zaidi karibu na tropiki. Kwa kawaida mayai ni meupe au yenye rangi ya maziwa, na kwa kawaida hung'aa.

Spishi za Afrika

Spishi za mabara mengine

Picha

license
cc-by-sa-3.0
copyright
Waandishi wa Wikipedia na wahariri

Hinabuluu: Brief Summary ( Swahili )

provided by wikipedia emerging languages

Hinabuluu ni ndege wa ardhi wa familia Pittidae. Ndege hawa ni wakubwa na wanene kiasi wenye miguu mirefu, mkia mfupi sana na domo lenye nguvu. Spishi nyingi zina rangi kali. Wanatokea ardhini kwa misitu minyevu ya tropiki ya Afrika, Asia na Australia. Hula makoa, wadudu na wanyama wengini kama wale. Hujenga tago la mviringo kwa manyasi na majani lenye mwingilio kwa upande wake. Jike huyataga mayai 4-5.

license
cc-by-sa-3.0
copyright
Waandishi wa Wikipedia na wahariri